Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Mhandisi Paskasi Muragili akizungumza na Maafisa Lishe, Wakuu wa Idara na Watendaji wa Kata katika kikao kazi cha Lishe kilichofanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida. Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Muragili amewaagiza Maafisa Lishe wakishirikiana na Watendaji wa Kata na viijiji kuhakikisha elimu ya Lishe bora inawafikia wananchi wote, kwani lishe bora hujenga afya bora na kwa kuzingatia ulaji bora jamii itaepukana na changamoto za udumavu wa akili kwa watoto na hivyo kuleta tija katika ufaulu wa wanafunzi mashuleni.
Akitolea taarifa juu ya hali ya lishe mashuleni, mwalimu Juma Sabigoro (wa tatu toka meza kuu) kwa niaba ya Afisa Elimu Wilaya ameelezea kuwa kakribani shule zote za Halmashauri ya Wilaya ya Singida zinapata Lishe kwa kuanzia na kifungua kinywa cha uji. Mwalimu Sabigoro ameongezea kwa kusema hata hivyo jitihada zinaendelea kufanywa na bodi za shule kuendelea kuhimiza wazazi wa wanafunzi umuhimu wa kuchangia chakula mashuleni ili watoto wao waweze kupata lishe bora na hivyo kuchangia ufaulu wa mwanafunzi huyo. Mwalimu huyo ameongezea na kusema kuwa takribani shule zote zenye maeneo ya kilimo wamehakikisha yamelimwa ili kuongezea uwezo wa shule kulisha wanafunzi wake na hivyo kuwa na afya bora.
Akitoa taarifa jumuishi ya lishe Mratibu wa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Bi: Neema Swai ameelezea kuwa kwa kipindi cha robo ya kwanza na robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/ 2023 huduma ya Lishe kwa mama mjamzito na mtoto imeendelea kuboreshwa katika vituo vya afya 40 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ambapo idadi ya wakina mama wanaojifungulia majumbani imepungua kutoka wakina mama193 hadi wakina mama 89. Huduma za utoaji wa chanjo ya mama na mtoto pamoja na kinga ya malaria dhidi ya mama mjamzito imeendelea kutolewa kwa kushirikiana na Watoa Huduma Ngazi ya Jamii. Wataalamu wa afya wameendelea kutoa elimu juu ya matumizi ya chumvi yenye madini joto kwani ina mchango mkubwa katika lishe bora, hata hivyo asilimia 57.3 ya chumvi inayotumika katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ina madini joto. Afisa Lishe huyo ameongezea kusema kuwa jitihada jumuishi zinahitajika katika kuendelea kutoa elimu katika jamii juu ya umuhimu wa mzazi kujifungua katika kituo cha afya ili kutokomeza kabisa vifo vya mama na mtoto.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Mhandisi Paskasi Muragili ametoa onyo kuwa ni marufuku kwa mama mjamzito kujifungulia nyumbani na endapo taarifa itatolewa ya mzazi aliyejifungua nyumbani maelezo ya kina waweze kutolewa na Mtaalamu wa Afya kuwa ni mazingira gani yaliyopelekea tukio hilo. Akiongea na Watendaji wa Kata, Vijiji na Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Mkuu huyo wa Wilaya amekemea vikali tabia za baadhi ya walimu mashuleni kuuza au kutumia chakula cha shule, au mazao yatokanayo na shamba la shule kwa maslahi yao binafsi.
Mhe. Muragili ameendelea kusisitiza Maafisa Lishe na Watendaji wakishirikiana na Watoa Huduma Ngazi ya Jamii kuendelea kutoa elimu katika jamii juu ya umuhimu wa Lishe bora, pia matumizi ya chumvi yenye madini joto na kuagiza Wataalamu wa Lishe kupiga marufuku na kukamata chumvi zinazoingizwa sokoni zisizo na madini joto kwani ukosefu wa madini joto katika mwili wa binadamu una madhara katika afya ya jamii.
Ilongero
Anuani ya Posta: Box 27, Singida
Simu: +25526502252
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded.singidadc@singida.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Singida. Haki zote zimehifadhiwa.